Google Ya Mafanikio
Ongea Na Kocha.
Ongea Na Kocha; Kisima, Tathmini, Rejoyce Otaru.
0:00
-3:19:17

Ongea Na Kocha; Kisima, Tathmini, Rejoyce Otaru.

ONGEA NA KOCHA; KISIMA, TATHMINI, REJOYCE OTARU.

Karibu mwanamafanikio kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kina mambo makubwa manne ya kujifunza kwenye safari yetu ya mafanikio.

Jambo la kwanza ni mambo ya muhimu na ya msingi ya kuzingatia kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Kwa sasa tunapotia mageuzi makubwa kwenye KISIMA kutoka kuwa kundi la kujifunza na kwenda kuwa jumuia za wanamafanikio. Katika mageuzi haya KISIMA kinataka kila mmoja kujitoa zaidi ili kuweza kufanikisha lengo la pamoja ambalo wote tunalo. Nimeshirikisha dhana nzima ya KISIMA CHA MAARIFA NI JESHI, adui yetu mkuu tunayemkabili na ushindi ambao tunataka kuupata.

Jambo la pili ni mrejesho wa tathmini za mwezi Februari 2022. Baada ya kupitia na kujibu tathmini za wanamafanikio kwa mwezi Februari 2022 nimekusanya mambo 11 ambayo nimetoa ufafanuzi kwa wote. Ni mambo ya msingi sana kama kujenga wateja 100 wa uhakika, mahusiano ya ndoa na mafanikio, kutokutetereshwa na misukumo ya kifamilia na kijamii na mengine mengi. Ni mambo muhimu kusikiliza na kujifunza ili kuweza kuendelea na safari ya mafanikio kwa ushindi mkubwa.

Jambo la tatu ni mahojiano na mwanamafanikio mwenzetu Rejoyce Otaru ambaye anaendesha biashara ya mgahawa wa chakula uliopo Morogoro. Kupitia mahojiano hayo Rejoyce anashirikisha changamoto kubwa anazokabiliana nazo kwenye biashara yake ambazo ni mtaji, wateja, mauzo na timu. Anatueleza kwa kina namna anavyopambana kukabiliana na changamoto hizo ili biashara yake iweze kuvuka na kufikia mafanikio makubwa. Mahojiano haya yana mafunzo mengi sana kuanzia kuanza biashara na katika kuiendesha.

Jambo la nne ni mjadala wa wanamafanikio wote, ambao kwa kiasi kikubwa wametoa ushauri mzuri mno kwa Rejoyce kwa namna anavyoweza kukabiliana na changamoto zake za kibiashara. Ushauri umeanzia kwenye kujitambua yeye mwenyewe kwa uimara na madhaifu yake, kuzingatia misingi muhimu ya biashara ya mgahawa na kutengeneza wateja wa uhakika kulingana na uwezo tofauti tofauti wa wateja. Ameshauriwa pia kuhusu kudhibiti gharama za biashara, kuboresha huduma na kujenga timu. Kuna mengi mno ya kujifunza kutoka kwenye ushauri ambao wanamafanikio wamempa mwenzetu Rejoyce.

Rafiki, tenga muda usikilize kipindi hiki cha ONGEA NA KOCHA, na unaposikiliza kuwa na kijitabu chako ili uandike yale unayojifunza na uende kuyafanyia kazi kwenye safari yako ya mafanikio.

Nikutakie kila la kheri na karibu sana tuendelee kuwa pamoja kwenye safari hii ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Kocha.

0 Comments
Google Ya Mafanikio
Ongea Na Kocha.
Karibu kwenye vipindi vya sauti vya Ongea Na Kocha ambapo Kocha Dr Makirita Amani atakuwa anakushirikisha maarifa mbalimbali ya mafanikio pamoja na kujibu maswali na changamoto unazokutana nazo kwenye safari yako ya mafanikio.