Google Ya Mafanikio
Ongea Na Kocha.
Ongea Na Kocha; Instant Cashflow – Kuongeza Idadi Na Kiwango Cha Manunuzi.
0:00
-3:07:35

Ongea Na Kocha; Instant Cashflow – Kuongeza Idadi Na Kiwango Cha Manunuzi.

Habari Mwanamafanikio?

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumeendelea na uchambuzi wa kitabu cha INSTANT CASHFLOW kilichoandikwa na Bradley Sugars.

Kitabu hiki ni mwendelezo wa msingi mkuu tuliojifunza kwenye kitabu cha BILLIONAIRE IN TRAINING cha mwandishi huyo huyo.

Kwenye BILLIONAIRE IN TRAINING tulijifunza ngazi tano za ujasiriamali ambazo ni kama ifuatavyo;

Ngazi sifuri; mwajiriwa, hapa chanzo cha kipato ni ajira tu.

Ngazi ya kwanza; kujiajiri, hapa unafanya kila kitu mwenyewe.

Ngazi ya pili; meneja, hapa umeajiri wengine kukusaidia, ila bila uwepo wako hakuna kinachoenda.

Ngazi ya tatu; uongozi, hapa biashara inaweza kwenda bila uwepo wako.

Ngazi ya nne; uwekezaji, hapa unanunua, kujenga na kuuza biashara mbalimbali.

Ngazi ya tano; mjasiriamali, hapa unaingiza kampuni kwenye soko la hisa au kuuza leseni na wengine kuweza kuendesha biashara yako na kukulipa.

Kitu kingine kikubwa tulivyojifunza kwenye kitabu cha BILLIONAIRE IN TRAINING ni injini kuu ya ukuaji wa biashara. Tumejifunza matokeo matatu yanayopimwa kwenye biashara, ambayo ni WATEJA, MAUZO na FAIDA.

Ili kupata matokeo hayo matatu, kuna vitu vitano vya kufanya, ambavyo ndiyo vimejadiliwa kwa kina kwenye kitabu cha INSTANT CASHFLOW. Vitu hivyo vitano ni kama ifuatavyo;

Moja; kufikia wateja tarajiwa.

Mbili;  kuwashawishi wateja hao wanunue.

Tatu; kuwafanya wateja warudi kununua.

Nne; kuwafanya wateja wafanye manunuzi kwa wingi.

Tano; kuongeza kiwango cha faida.

Kwenye sehemu ya uchambuzi uliopita, ambayo inapatikana hapa, tuliangalia sehemu mbili za kwanza, kufikia wateja na kuwashawishi.

Kwenye sehemu hii ya uchambuzi tunaangalia sehemu nyingine mbili, kuongeza idadi na kiwango cha manunuzi.

Na sehemu ya mwisho ya uchambuzi wa kitabu hiki tutaangalia kuongeza kiwango cha faida.

Kitu kikubwa kabisa kutoka kwenye mjadala wa kipindi hiki ni pendekezo la kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kupanda ngazi za ujasiriamali kila mwaka wa mafanikio.

Wazo hili ni zuri na muhimu kabisa kwani ndiyo litatupeleka kwenye lengo letu kuu moja ambalo ni kufikia uhuru wa kifedha.

Kwa maana hiyo basi, tunaendelea kuboresha mkakati wetu wa KISIMA CHA MAARIFA ambao unakwenda kuwa kama ifuatavyo;

Kwenye mwaka wa mafanikio 2021/2022; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya kwanza ya ujasiriamali, yaani kujiajiri. Hata kama umeajiriwa, unapaswa kuwa na biashara ya pembeni yenye wateja ambao unawahudumia wewe mwenyewe moja kwa moja.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2022/2023; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya pili ya ujasirimali, yaani kuwa na biashara yenye wasaidizi, hata kama bado inamtegemea kwa kila kitu. Idadi yoyote ya wafanyakazi ni sawa, muhimu ni usiwe unafanya mwenyewe kila kitu. Na hii ndiyo hatua ya kuandaa na kuanza kutumia mfumo wa biashara.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2023/2024 na 2024/2025; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya tatu ya ujasiriamali, yaani ana biashara inayojiendesha yenyewe bila ya kutegemea uwepo wake moja kwa moja. Hii ndiyo hatua ya kuanza kupata uhuru wa muda na fedha. Ngazi hii tunaipa miaka miwili kwa sababu ina kazi kubwa ya kufanya ndani yake. Lakini katika kukamilisha miaka hiyo miwili, hakuna anayepaswa kuwa anategemewa na biashara moja kwa moja.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2025/2026 na 2026/2027; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya nne ya ujasiriamali, yaani kununua, kujenga na kuuza biashara mbalimbali au kuwa na biashara zaidi ya moja zinazojiendesha zenyewe na kuweza kuziuza. Kwenye hatua hii ongezeko la kipato linakuwa kubwa huku uhuru ukizidi kuongezeka. Ngazi hii pia miaka miwili kwa sababu ina kazi kubwa ya kufanya.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2027/2028 mpaka 2029/2030; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa amefikia ngazi ya tano ya ujasiriamali ambayo ndiyo ujasiriamali kamili. Katika ngazi hii kila mmoja anakuwa ameweza kufikisha kampuni kwenye soko la hisa au kuuza leseni kwa wengine kuendesha na wakamlipa. Hatua hii ina miaka mitatu kwa sababu ina mchakato mkubwa wa kisheria wa kufuata ili kuikamilisha.

Kwa mkakati huu, tunapokwenda kufika mwaka 2030 kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anakuwa amefikia uhuru kamili wa fedha, muda na maisha na kuendelea kufanyia kazi ndoto zake nyingine alizonazo.

Mkakati huu ni kwa upande wa biashara, mikakati ya uwekezaji itakuwa inaendelea kwa kila mwaka na hapa tutatengeneza viwango vya uwekezaji vya kila mwanachama kuwa amefikia kwenye kila mwaka.

Maeneo ya kuwekeza na kiwango cha kufikia kila mwaka mpaka kufika mwaka 2030 tutavijenga na kushirikishana.

Swali kubwa ambalo wengi wanaweza kuwa nalo ni vipi kama mtu atashindwa kufikia kiwango kwa mwaka husika?

Jibu lipo wazi, anakuwa amekosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA.

Jambo muhimu la kujua ni kwamba muda tuliojiwekea ni mrefu na unamtosha kila mtu hata mwenye kasi ndogo kiasi gani. Hivyo hakuna aliyedhamiria kweli ambaye ataachwa nyuma. Lakini kwa kwenda kwa mazoea, lazima utaachwa nyuma.

Karibu usikilize kipindi cha ONGEA NA KOCHA kujifunza yale muhimu kutoka kwenye kitabu na safari ya mafanikio.

Kocha.

0 Comments
Google Ya Mafanikio
Ongea Na Kocha.
Karibu kwenye vipindi vya sauti vya Ongea Na Kocha ambapo Kocha Dr Makirita Amani atakuwa anakushirikisha maarifa mbalimbali ya mafanikio pamoja na kujibu maswali na changamoto unazokutana nazo kwenye safari yako ya mafanikio.