Google Ya Mafanikio
Ongea Na Kocha.
ONGEA NA KOCHA; Miminalist Entrepreneur, Tathmini Ya Robo Mwaka, Changamoto Ya Siku 100.
0:00
-3:08:00

ONGEA NA KOCHA; Miminalist Entrepreneur, Tathmini Ya Robo Mwaka, Changamoto Ya Siku 100.

Habari mwanamafanikio?

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo kuna mambo makubwa matatu.

Moja ni uchambuzi wa kitabu kinachoitwa MINIMALIST ENTREPRENEUR kilichoandikwa na Sahil Lavingia.

Hiki ni kitabu ambacho Sahil ameshirikisha safari yake ya kujenga biashara kwa kuzingatia yale ya msingi badala ya kuhangaika na sifa zisizo na tija.

Kwenye kipindi hiki tumejadili mambo nane ya msingi ambayo Sahil ameshirikisha kwenye kitabu kama ifuatavyo;

1.       Msingi mkuu wa kuzingatia kwenye biashara ni THAMANI na FAIDA. Toa thamani kwa wateja na hakikisha biashara inaingiza faida.

2.       Anza na jumuia uliyopo. Waangalie wale wanaokuzunguka na matatizo waliyonayo kisha njoo na suluhisho la matatizo hayo.

3.       Jenga kidogo iwezekanavyo. Baada ya kujua suluhisho linalowafaa wateja, usikimbilie kufanya uwekezaji mkubwa mwanzoni, bali fanya yale ya msingi ya kumwezesha mteja kupata thamani na biashara ikapata faida.

4.       Uza kwa wateja 100 wa kwanza. Hapa anza na wale unaowajua au unaoweza kuwafikia na kuwaelimisha kuhusu kile unachouza.

5.       Fanya masoko na uwafikie wateja wengi zaidi na usitumie gharama kubwa. Tumia maudhui kufundisha, kuhamasisha na kuelimisha wateja tarajiwa ili wajenge uaminifu na kushawishika kununua.

6.       Kua kwa umakini. Kwa kuzingatia hatua hizo nyingine, biashara itakua. Wakati wa ukuaji ni wakati wenye hatari kubwa kwa biashara kufa kwa kupoteza fedha, nguvu na timu. Unapaswa kuwa makini ili hayo yasitokee kwenye ukuaji.

7.       Jenga nyumba unayotaka kuishi. Tengeneza maono ya biashara yako, weka misingi, sheria na taratibu mbalimbali na weka maadili ambayo kila mtu anayasimamia. Kwa njia hiyo utaweza kuajiri watu sahihi na kuwa na utamaduni mzuri kwenye eneo lako la biashara.

8.       Fikia uhuru kamili wa maisha yako na fanya kile unachotaka. Kwa kuijenga biashara vizuri, itafika hatua ambayo haikuhitaji tena, inaweza kujiendesha bila ya uwepo wako. Hapo ndipo unakuwa umefikia uhuru kamili na kuweza kufanya yale unayopenda na kujali zaidi.

Hayo ndiyo mambo ya msingi kabisa ya kujifunza kutoka kwenye kitabu cha MINIMALIST ENTREPRENEUR ambapo kwenye kipindi hiki nimeyaelezea kwa kina zaidi.

Jambo la pili ni mwongozo wa kuandaa TATHMINI YA ROBO MWAKA kwenye mwaka wetu wa mafanikio 2021/2022. Hili ni zoezi muhimu kwenye KISIMA CHA MAARIFA ili kuweza kupima kile ambacho tunafanya kulingana na malengo ambayo tunayo. Kwenye kipindi nimeshirikisha mwongozo mzima wa kukamilisha hilo.

Jambo la tatu ni CHANGAMOTO YA SIKU 100 inayokwenda kuanza juma la 16. Ni siku 100 za kuchagua kufanya kitu kila siku bila kuacha na kuonyesha ushahidi. Kwenye kipindi nimeeleza kuhusu changamoto hiyo na mambo muhimu ya kuzingatia.

Karibu sana usikilize kipindi hiki cha ONGEA NA KOCHA ili uweze kujifunza na kuondoka na mambo ya kwenda kufanyia kazi ili kufika kwenye maono na ndoto zako kubwa.

Kocha.

0 Comments