“If you shape your life according to nature, you will never be poor. If you shape your life according to people’s opinions, you will never be rich.” – Epicurus
Ukiyaendesha maisha yako kulingana na asili, kamwe huwezi kuwa masikini.
Kwa sababu asili inataka mambo machache sana na ambayo yako ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu, bila ya kujali yupo kwenye hali gani.
Ukiyaendesha maisha yako kulingana na maoni ya wengine, kamwe hutakuwa tajiri.
Kwa sababu maoni ya wengine hayana ukomo, hata uwe na nini, kuna wengine watakuwa na zaidi yako.
Asubuhi ya leo tafakari ni mara ngapi umejitesa kwenye maisha ili tu uwe kama watu wengine.
Mara ngapi umekopa vitu kwa sababu wengine wanavyo au wanakushangaa wewe huna.
Kama utaendelea kuishi maisha yako kwa namna hiyo, kila siku utakuwa mtumwa wa wengine.
Kwa hatua yoyote uliyopo sasa kwenye maisha, chagua kuyaishi maisha yako.
Fanya mambo kwa sababu ni muhimu kwako na yana maana kwako, siyo kwa sababu kila mtu anafanya au unataka uonekane unafanya.
Hii haimaanishi uridhike na machache, unapaswa kupiga hatua kadiri uwezavyo, lakini siyo kwa kusukumwa au kujilinganisha na wengine.
Chagua kuyaishi maisha yako kulingana na asili na yatakuwa bora na tulivu bila ya kujali yakoje.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu maisha kwenda kama unavyotaka wewe, soma hapa; www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/29/2129
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Asante Kocha kwa tafakari njema. Nachagua kuishi maisha yangu bila kujali yapo kwenye hali gani