#TAFAKARI YA LEO; HAMASA NA KIPAJI PEKEE HAVITOSHI...
"As habit is more dependable than inspiration, continued learning is more dependable than talent." -- Octavia Butler
Ili kuanza kufanya kitu, unahitaji kuwa na hamasa ndani yako ya kukifanya.
Lakini hamasa huwa haidumu, ni kitu cha muda mfupi tu.
Hivyo ili uendelee kufanya, unapaswa kujijengea tabia, ikishakuwa tabia, inakuwa rahisi kuendelea kufanya.
Ukisema usubirie mpaka upate hamasa ndiyo ufanye hutaweza kufikia mafanikio makubwa.
Jijengee tabia kwenye kile unachofanya na utaweza kukifanya kila wakati, iwe una hamasa au la.
Ili ufanye kitu vizuri, unahitaji kuwa na kipaji fulani kwenye kitu hicho.
Lakini kipaji hicho kitakupa mafanikio ya mwanzo tu, ili uendelee kufanya makubwa na kufanikiwa zaidi, lazima uendelee kujifunza kila wakati.
Haijalishi una kipaji kiasi gani, kama huendelei kujifunza, unajiwekea ukomo kwenye mafanikio unayoweza kufikia.
Kujifunza kila wakati kunakupa fursa ya kujua zaidi na kuweza kufanya zaidi.
Asubuhi ya leo tafakari ni jinsi gani umekuwa unachukulia mambo hayo mawili. Jiulize kama umeshajijengea tabia kwenye yale muhimu unayofanya au umekuwa unasubiria tu hamasa.
Pia jiulize ni kwa kiasi gani umekuwa unaendelea kujifunza hata yale unayoamini una kipaji katika kuyafanya.
Kujijengea tabia kwenye yale unayofanya na kuwa mtu wa kujifunza kila wakati, itakufikisha kwenye mafanikio makubwa kuliko kutegemea hamasa na kipaji pekee.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kutumia muda ili kuokoa pesa, soma hapa; www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/31/2131
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.